Tuesday, 6 December 2016

KATIBU TAWALA MKOA WA MOROGORO AITAMANI MOROGORO YA ZAMANI.

                       

      Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Dr. John Ndunguru amesema Mkoa wa Morogoro umebarikiwa kuwa ni kitovu cha wanamichezo  na kutaka hali hiyo kurejeshwa kwa kuwa Morogoro sasa ni  Mkoa  ambao uko salama.
Dkt. Ndunguru ametoa wito huo mwishoni mwa wiki akimwakilishi Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe ambaye alialikwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuhitimisha mashindano ya magari ya siku mbili  yaliyofanyika Mkoani hapa ambapo pia alitoa zawadi mbalimbali kwa washindi wa mashindano hayo.
Dkt. Ndunguru amesema, Mkoa wa Morogoro una historia mbalimbali ikiwa ni pamoja na Morogoro ni Mkoa wa Viwanda na kitovu cha wanamichezo na hivyo akawataka vijana kutokaa vijiweni na kujihusisha na mambo yasiyofaa, badala yake wajihusishe na michezo.
“Vijana acheni kwenda vijiweni badala yake mjihusishe na michezo ili kuendeleza sifa ya Mkoa wa Morogoro kuwa kitovu cha michezo” alisema Dkt. Ndunguru.
Kiongozi huyo ngazi ya Mkoa alisema, aliipongeza timu ya soka ya Polisi Mkoa wa Morogoro kwa kuendelea kufanya vizuri pamoja na timu nyingine huku akisema ana imani sasa Morogoro itakuwa kama zamani  yaani kuwa kitovu cha wanamichezo.
Aidha, Dkt. Ndunguru alitumia fursa hiyo kuwaalika Watanzania na wafanya biashara wengine kutoka ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza Morogoro kwa kuwa ni moja ya Mikoa ambayo ni tulivu, salama na inafaa kwa kilimo na shughuli nyingine za kiuchumi.
Akiwatoa wasiwasi wanaotaka kuwekeza Morogoro, Dkt. Ndunguru alisema,  kwa sasa Mkoa wa Morogoro uko salama na kwamba migogoro iliyokuwa inatokea siku za nyuma na kusababisha mapigano kwa baadhi ya maeneo, migogoro hiyo imekwisha na sasa Mkoa unaendelea kusisitiza suala nzima la Uwekezaji.
Awali, mwenyekiti wa Mashindano ya magari,  Clabu ya MOUNT ULUGURU RALLY ya Morogoro Dr. Mosi Makau, alibainisha kuwa mashindano hayo ni awamu ya nane kwa mwaka huu, walioshiriki ni madereva 11, jumla ya magari matatu yalipata hitilafu wakati wa mashindano na hivyo madereva wanane ndiyo waliofaulu kukamilisha mashindano hayo


By John jbp

No comments: