Thursday, 1 December 2016

Wanafunzi zaid ya nusu wachaguliwa kuingia kidato cha kwanza.


Dar/Mikoani. Zaidi ya nusu ya wanafunzi waliofaulu mitihani ya darasa la saba wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza huku wengine wakibaki kutokana na kukosa nafasi.

Dar es Salaam
Jumla ya wanafunzi 32,668 kati ya 51,488 waliofaulu mtihani wa darasa la saba katika Mkoa wa Dar es Salaam wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2017.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresia Mmbando alisema waliofanya mtihani huo mwaka huu walikuwa 62,346 sawa na asilimia 99.28 na watahiniwa 450 sawa na asilimia 0.73 hawakufanya kutokana na sababu mbalimbali na wanafunzi 18,820 wamekosa nafasi.
Alisema wanafunzi zaidi ni 72 wamechaguliwa kujiunga na shule za ufaulu mzuri na waliochaguliwa kwenda shule za ufundi ni 80.
Waliochaguliwa nafasi za kwanza zimeongozwa na Shule ya Tusiime ambako wavulana tisa kati ya 10 na wasichana saba kati ya 10 wametoka katika shule hiyo.
Alisema shule za mkoa zimechukua wanafunzi 1,720 na 30,654 wamechaguliwa kujiunga na sekondari za wananchi.
Hata hivyo, alisema kuna nafasi 1,246 katika shule za pembezoni mwa mji/vijijini ambazo zimebaki wazi na wanafunzi waliobaki wanategemewa kuchaguliwa kuzijaza katika awamu ya pili.

Mwanza
Katika mkoa huo, wanafunzi 43,536 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza sawa na asilimia 99.5.
Ofisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Hamisi Maulidi alisema kati wanafunzi hao, 294 sawa na asilimia 0.5 hawakufanya mtihani huo kwa sababu za vifo, ugonjwa, mimba na uhamisho huku 54 wakifutiwa matokeo.
Wilaya ya Ukerewe iliyokuwa ya kwanza mwaka jana, imekuwa ya mwisho kati ya wilaya nane za mkoa huo.
Nyamagana imeongoza ikifuatiwa Ilemela, Buchosa, Magu, Sengerema, Kwimba na Misungwi huku shule nne kati ya 10 bora zenye wanafunzi zaidi ya 40 zikitoka Ilemela.
Maulidi aliagiza wanafunzi wote watakaoandikishwa kidato cha kwanza wapimwe uwezo wao kitaaluma na wasiokidhi vigezo waondolewe.

Pwani
Mkoani Pwani, wanafunzi 9,290 kati ya 24,818 waliofanya mtihani huo wamefeli na hivyo kupoteza sifa ya kujiunga na elimu ya sekondari.
Idadi hiyo ni sawa na asilimia 37.43 ya watahiniwa wote 24,818 waliofanya mtihani huo. Wengine 95 sawa na asilimia 0.38 hawakufanya mitihani kutokana na sababu mbalimbali wakiwamo 75 watoro, mimba (1), vifo (11), ugonjwa (2) na sababu nyingine (6).
Kaimu Ofisa Elimu Pwani, Modest Tarimo alisema mkoa huo umechagua wanafunzi 15,528 kati ya 24,818 waliofanya mtihani huo kujiunga na sekondari kwenye shule za Serikali.
Alisema ufaulu huo hauridhishi kwani haujafikia kiwango kilichowekwa na Serikali cha asilimia 80 kwa mujibu wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN). “Wanafunzi 15,528 wamefaulu na kupata alama zaidi ya 100, kati yao 288 wamepata daraja A, 2,636 daraja B na 12,604 daraja C na hao ndiyo wamechaguliwa kuendelea na sekondari.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo, Edward Mwakipesile alisema mpango wa elimu bure umeongeza idadi ya wanafunzi hivyo wakuu wa wilaya, wenyeviti wa halmashauri na wakurugenzi wanatakiwa wakasimamie ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuwajengea mazingira mazuri wanafunzi hao.
Ameagiza wanafunzi waliopangiwa sekondari waripoti kwa wakati ili kusiwepo na atakayeachwa masomo yanapoanza na atakayeshindwa mzazi wake atawajibika.
“Hatutarajii hawa watoto waliopangiwa kwenda sekondari eti wakaachwa nyumbani, nawaagiza ninyi wajumbe mkashirikiane na viongozi ngazi za vijiji, mitaa na kata kuhakikisha wote wanakwenda shule,” alisema Mwakipesile.

Songwe
Katika mkoa mpya wa Songwe, zaidi ya wanafunzi 1,460 waliofaulu mtihani wa darasa la saba hawatajiunga na kidato cha kwanza kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa katika halmashauri za Mbozi na Mji wa Tunduma.
Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, Elia Ntandu alisema halmashauri hizo zina upungufu wa vyumba 36 vya madarasa.
“Natoa wito kwa halmashauri kuhakikisha ifikapo Machi 15 vyumba vyote vya madarasa vikamilike na wanafunzi hao waanze masomo,” alisema Ntandu.
Kaimu ofisa elimu mkoani hapa, Samweli Mshana aliwataka wadau na halmashauri kukamilisha haraka ujenzi wa vyumba vya madarasa ili watoto hao wasikate tamaa ya kuendelea na shule kutokana na kukaa nyumbani muda mrefu.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Jakaya Kikwete iliyopo wa Tunduma, Mostake Sambo alisema kukosekana kwa vyumba vya madarasa ni udhaifu wa jamii kutojiandaa kuwapatia elimu watoto.
Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka alisema halmashauri yake itakamilisha ujenzi huo kabla ya Machi

By John jbp

No comments: