ZIMEBAKI siku 36 mwaka 2016 umalizike. Yanga inaanza mazoezi Jumatatu wiki ijayo ikiwa chini ya kocha wao mpya George Lwandamina atakayetambulishwa rasmi kwa waandishi wa habari wakati wowote kutoka leo na ametema mkwara mzito.
Lwandamina amesema mafanikio yote anayoyapata sasa katika soka yanatokana na kuwa na misingi na misimamo imara na hataki kuyumbishwa.
“Unaweza kukuta mchezaji anapenda vita ya kupambana na mwenzake wa timu pinzani, nafikiri nyema akafanya hivyo kwa kutumia kipaji chake cha kucheza vizuri zaidi yake lakini ukipigana au kuanza kulumbana na waamuzi ni kitu ambacho sikipendi, kama kuna tatizo la mwamuzi aachiwe nahodha huyo ni badala ya yangu uwanjani,”alisema Lwandamina na kusisitiza kwamba hapendi wachezaji wake wale vitu vya mafuta wala wanga mwingi.
“Najua kuna tabia za wachezaji wale wanaoshindwa siku zote wamekuwa na tabia za ushawishi kwa kutengeneza makundi pembeni nikimtambua mtu wa namna hiyo nitamuondoa haraka na ikitokea akarudishwa naweza hata kuondoka mimi huyo ni mtu hatari na hili sio kwa mchezaji tu hata watu nitakaofanya nao kazi.
“Mimi ni kocha muhimu kwangu si ushindi wa mechi moja tunahitaji ushindi wa kombe sasa unapokutana na timu yenye wachezaji wanaotaka kucheza kwa kufurahisha mashabiki hao sio watu ninaowahitaji mashabiki wanataka makombe,”alisema na kuongeza hataki pia wachezaji wabaguane wala hataki kuwepo mkubwa wala mdogo.
“Ukianza kubagua wachezaji kwa kumuona mmoja ni bora kuliko mwingine ni wazi hapo umeharibu timu kama kuna mchezaji anajiona ni muhimu si katika timu yangu, kila mchezaji aliye katika kikosi changu ana umuhimu sawa kama mwingine.
“Duniani kuna wachezaji wawili tu wenye ubora wa dunia ambao ni Messi (Lionel) na Ronaldo (Cristiano) lakini acha mbali na ustaa wao bado wanafanya mazoezi makali tena zaidi ya wenzao na bado hawana majivuno nitawapa mfano wa huyu Mtanzania Sammata (Mbwana) yuko wapi sasa? Unafikiri kwanini amefanikiwa angekuwa na maringo sasa angekuwa ameshapotea..”
Beki huyo wa zamani wa Zambia alisema: “Unaweza kukuta mchezaji anapenda kuwa na visingizio anakwenda nyumbani au timu ya taifa kisha anachelewa kurudi niliwahi kumfukuza mchezaji mmoja wa Kenya kwa tatizo hilo nataka kufanya kazi na watu wanaoweka nyuma visingizio na kutambua klabu inamuhitaji ndiyo maana inamlipa fedha nyingi.”
Kocha huyo ametamka hayo huku akisisitiza nidhamu ya mazoezi pamoja na mchezaji kujiheshimu na kupunguza starehe siku za kazi. “Nahitaji kufanya kazi na wachezaji wanaojitambua tukifanya mazoezi fulani yaweke kichwani hicho ndicho ninachotaka ukifanye uwanjani ukishindwa hapo tambua umeshindwa kuitetea timu unaweza kujikuta unapoteza nafasi yako.”
“Napenda kuwa na vipindi vitano vya nguvu na vyenye ufanisi vya mazoezi kwa wiki nzima, nitaangalia hilo na wasaidizi wangu na sitaki kuona mchezaji mvivu katika eneo hilo kwani timu inajengwa hapo. Nahitaji kuwa na wachezaji wanaopendana na sio kutengana tukipendana na kuwa kitu kimoja kwa kuelekezana kwa taratibu hilo litatusaidia kama hakuna upendo hakuna mafanikio.
“Kama tukisema tukutane saa sita mchana basi kila mmoja awe pale lakini sio huyu yupo yule hayupo, ni vizuri kila mtu akajua kupangilia muda nitafurahi kuwa na wachezaji wa namna hiyo,”alisisitiza kocha huyo ambaye jukumu lake la kwanza ni kufufua matumaini ya Yanga kutetea ubingwa huku akijiandaa na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.
By john jbp
No comments:
Post a Comment