Friday, 25 November 2016

Mzee wa upako matatizoni



         Dar, Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) la Ubungo jijini hapa, Anthony Lusekelo ameingia matatani na vyombo vya dola kutokana na kudaiwa kumfanyia vurugu jirani yake.
Habari zinasema tukio hilo lilitokea juzi alfajiri na mitandao ya kijamii ilikuwa na picha zinazomuonyesha mchungaji huyo  akirushiana maneno makali na jirani huyo.
Mchungaji Lusekelo hakuweza kupatikana kuzungumzia sakata hilo, lakini mkewe alisema mtumishi huyo wa Mungu hakuwa mikononi mwa Jeshi la Polisi kama habari zilivyoenea awali.
Taarifa za kukamatwa kwa kiongozi huyo wa kiroho zilisambaa jana baada ya mwandishi wa habari(jina tunalihifadhi) aliyeshuhudia tukio hilo, kuandika kwa urefu kisa hicho na kusambaza kwenye mitandao ya kijamii.
“Mimi ndio nimeandika hilo tukio, nilishuhudia kisa hicho asubuhi ya jana (juzi) na ilipofika saa kumi alfajiri leo (jana) niliandika tukio hilo. Nilikuwa natakiwa kwenda ku-defend (kutetea) utafiti wangu katika Chuo Kikuu cha Bagamoyo, hata sielewi kwanini niliamua kupita maeneo hayo saa kumi na moja alfajiri wakati nilitakiwa kuwa chuoni saa nne asubuhi, nadhani Mungu alinituma,” alisema.
Picha ya video iliyosambaa mitandaoni jana inamuonyesha mtu anayedaiwa kuwa ni Mchungaji Lusekelo akijibizana na sauti ya mwanamke, ambaye haonekani, huku gari la rangi nyeusi aina ya Toyota Landcruiser likiwa limeegeshwa katikati ya barabara ya mtaani na kuzuia mengine kupita.
Mtu huyo anayedaiwa kuwa Mzee wa Upako, anaonekana amevalia shati la rangi ya bluu na suruali nyeusi, anasikika akimfokea mtu aliye ndani na kumuonya asikutane naye.
Mwandishi aliithibitishia blogu yetu kuwa taarifa hiyo iliyosambaa kuhusu Mzee wa Upako ni yake na kwamba alimkuta mchungaji huyo asubuhi eneo la Kawe Beach anakoishi akiwa anawatolea maneno makali watu waliokuwa ndani ya uzio wa nyumba, akidai kuwa wanamdharau.
Alisema kwa mujibu  watu saba aliowakuta kwenye eneo la tukio, mchungaji huyo alikuwa akirejea nyumbani kwake asubuhi hiyo akionekana kutokuwa katika hali ya kawaida.
Lakini kabla ya kufika nyumbani alisimamisha gari lake mbele ya geti la nyumba ya jirani yake na kuanza kuwatolea maneno hayo kwa madai kuwa wamekuwa wakimkebehi yeye kuwa hafai kuwa mchungaji kwa sababu ni mlevi.
“Nilimsihi sana hadi saa moja asubuhi nikimwomba anisikilize, aache kutukana, kutoka katika eneo la nyumba ya watu kwa sababu yeye ni mtumishi wa Mungu anajidhalilisha ,” alisema mwandishi.
Mwandishi alisema mchungaji huyo hakumsikiliza.
Mwandishi wa habari,ambaye alidai kuwa wakati huo Mzee wa Upako hakuonekana kuwa katika hali nzuri, alikubali kwenda nyumbani.
Hata hivyo,  mwandishi alisema baada ya muda mfupi Mzee wa Upako alirudi kwenye nyumba hiyo na kuanza tena kutoa maneno hayo.
Mwandishi alisema kwa kuwa kulikuwa kumeshapambazuka taarifa zilianza kusambaa, askari wa kituo cha polisi cha Kawe walifika eneo hilo na kumchukua.
Lakini Kamanda wa Polisi wa Kinondoni, Suzan Kaganda alisema hana taarifa za kukamatwa kwa Mzee wa Upako.
Wakati taarifa zinadai kuwa baadaye alichukuliwa na askari wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamanda Simon Sirro hakutaka kuzungumzia suala hilo na kuahidi kutoa taarifa ya tukio hilo leo.
Mlinzi wa nyumba ambayo Mchungaji Lusekelo alikutwa akitoa maneno hayo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, akisema alifika asubuhi majira ya saa 11:00 na kuegesha gari barabarani kisha kuanza kufoka.
Baada ya kufoka mtu mmoja alitoka na kumuita kwa kutumia cheo cha mchungaji, lakini alijibiwa “mchungaji hukohuko”, na kuendelea kufoka, jambo lililofanya walinzi kupiga simu polisi.
Alisema polisi walifika muda mfupi baadaye na kutaka kujua sababu za mchungaji huyo kuitaarifu polisi kama ana matatizo na jirani yake, lakini akawa anatoa maelezo ambayo walishindwa kuyaelewa na hivyo kuondoka naye.
Mke wa mchungaji huyo, alikanusha taarifa hizo
“Mume wangu yupo nyumbani hapa. Hizo taarifa hazina ukweli wowote,” alisema.
Kuhusu madai ya kutoa maneno nayo, Ngasala alisema: “Hata huo waraka si wa kweli. Mchungaji hawezi kutoa maneno kama hayo.”
Ngasala, ambaye alithibitisha kwamba mume wake yupo nyumbani alipoombwa ampe Mzee wa Upako simu ili mwandishi azungume naye, alisema apigiwe kwenye simu yake.
Mwandishi alipomwambia kwamba mchungaji huyo amepigiwa simu yake lakini hajapokea, alisema mume wake hajakamatwa na kwamba kuna kinyozi alifika kwa ajili ya kumnyoa nywele, hivyo apigiwe baadaye.
                 

   By john jbp

No comments: